96.The Clot

  1. Soma, ewe Nabii, Qur’ani uliyoteremshiwa ukianza kwa Jina la Mola wako Aliyepwekeka kwa kuumba
  2. Aliyemuumba kila binadamu kwa pande la damu nzito nyekundu
  3. Soma, ewe Nabii, kile ulichoteremshiwa, na Mola wako ni Mwingi wa wema, Mwingi wa ukarimu
  4. Aliyewafundisha viumbe vyake kuandika kwa kalamu
  5. Alimfundisha binadamu vitu ambavyo hakuwa akivijua. Akamtoa kwenye giza la ujinga, Akampeleka kwenye nuru ya elimu
  6. Kweli, binadamu hukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu
  7. akijiona ametosheka kwa utajiri wake
  8. Basi, ajue kila mwenye kutupa mipaka kuwa mwisho atarudi kwa Mwenyezi Mungu Ambaye Atamlipa kila binadamu kwa alilolitenda
  9. Je, umeona ujeuri wa ajabu zaidi kuliko wa mtu huyu, Abu jahl
  10. Anayemkataza mja wetu, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, anapomsalia Mola wake
  11. Waonaje iwapo mwenye kukatazwa kusali yuko uongofuni, vipi anamkataza
  12. Au iwapo anaamrisha mwigine kumcha Mungu, vipi anamkataza hilo
  13. Waonaje iwapo huyu mwenye kukataza anakanusha lile alinganiwalo kwalo na kulipa mgongo
  14. hajui kuwa Mwenyezi Mungu anaona kila analolifanya
  15. Basi mambo si kama anvyodai Abu Jahl. Na asipokomeka na ushindani alionao na udhia wake, Tutamshika upaa wake kwa nguvu na kumtia Motoni
  16. Upaa wake ni upaa wenye maneno ya urongo na vitendo vya makosa
  17. Basi na awalete, mtupaji mipaka huyu, watu wa baraza ili wamsaidiye
  18. Sisi Tutawaita Malaika wa adhabu
  19. Mambo si kama Abu Jahl anavyoyadhania. Yeye, ewe Mtume, hawezi kukufanya lolote la kukudhuru Usimfuate kwa lile alilokuitia la kuwa uache Swala, bali msujudie Mola wako na uwe karibu na Yeye kwa kujipendekeza Kwake kwa kumtii